tororo-cementWaandishi wa habari wa Tanzania walipotembelea Kiwanda cha Saruji Tororo nchini Uganda ambako walijionea mkaa wa mawe unaotumiwa na kiwanda hicho kutoka nchini Afrika Kusini

KAMPENI chafu dhidi ya makaa ya mawe yanayopatikana nchini imevuka mipaka baada ya Kampuni ya Saruji ya Tororo nchini Uganda kutumia madai ubora kukwepa kuagiza kutoka Tanzania.

 

Kampuni hiyo huagiza tani 35,000 za makaa ya mawe kila mwaka kutoka nchini Afrika Kusini na tani zingine 35,000 za gypsum kutoka nchini Oman.

Malighafi yote hiyo, makaa ya mawe na gypsum, zinapatikana kwa wingi nchini na kutokana na ushirikiano wa kikanda uliopo wa nchi za Afrika Mashariki ilitegemewa nchi hiyo kutumia malighafi zilizoko ndani ya nchi wanachama.

Meneja Uzalishaji wa Kiwanda cha Saruji Tororo, Peter Karanja aliwaeleza waandishi wa habari za masuala ya ugatuzi kutoka Tanzania na Uganda, sababu za kuagiza bidhaa hizo kutoka nje ya nchi wanachama wa Shirikisho la Afrika Mashariki kuwa ni kutokana ubora hafifu wa makaa ya mawe yapatikanayo nchini.

Hata hivyo, wakati madai hayo yakisambaa hadi nchi jirani, baadhi ya viwanda saruji nchini, kikiwemo cha Mbeya vinatumia makaa ya mawe ya ndani na kuyaelezea kuwa na ubora wa hali ya juu.

“Mbeya Cement tunatumia makaa ya mawe toka Kampuni ya TAN Coal, na hatuoni tatizo lolote,” kinasema chanzo chetu kutoka ndani ya kampuni hiyo ambaye hata hivyo alisema yeye sio msemaji wa kampuni.

Mtaalamu huyo wa masuala ya saruji kiwandani hapo hakubaliani na suala la ubora kuwa kikwazo cha kutumia makaa ya hapa nchini akisema ubora wa makaa hautofautiani sana kwani yanapatikana kwenye mwamba wa aina moja.

maka-maweMkaa wa mawe toka Afrika Kusini unaotumiwa na Kiwanda cha Saruji Tororo. Swali ambalo halijajibiwa hadi sasa ni kwa nini watumiaji wakubwa wanakwepa mkaa toka nchini.

Meneja Udhibiti wa Ubora wa Makaa ya mawe, Kampuni ya TAN Coal, Bosco Mabena anathibitisha viwanda mbali mbali ndani na nje ya nchi kutumia makaa yao ya mawe kutoka Mgodi wa Ngaka.

Pamoja na Kiwanda cha Saruji Mbeya, Mbeya anavitaja viwanda vingine vinavyotumia mkaa wao kuwa ni viwanda vya saruji Tanga, Lake na Uniliver.

Mbena anazitaja nchi za Kenya na Rwanda kuwa nao baadhi ya viwanda vyao vinatumia makaa ya mawe kutoka mgodi huo wa Ngaka yanayochimbwa na kampuni yao.

“Hili suala la ubora ni siasa tu, halina ukweli, mimi ndiye na husika na udhibiti wa ubora wa makaa yam awe, uko vizuri,” alisema Mbena katika mahojiano yake kwa njia ya simu na mwandishi wa habari hii.

Anasema tofauti huchangiwa zaidi na manunuzi, ambako anasema kuna masuala ya bei na urasimu.

Mwanahabari nguli kutoka nchini Cameron, Eric Chinje analiangalia suala la masoko barani Afrika kama jambo la msingi lililopuuzwa.

Akitoa mada kuhusu vyombo vya habari na siasa barani Afrika, Chenje alisema niudhaifu mkubwa kutolitumia soko la ndani na kubabaika na bidhaa toka nje ya bara hili na kuitaja kuwa moja ya hatua zinazodhoofisha uchumi wa nchi za Kiafrika.

“Nchi za Kiafrika zinatakiwa kuungana na kulitumia soko la ndani lenye watu zaidi ya milioni 500,” alisema Chenje.